5:47 PM
Dj Brian
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari
Matui wilayani Kiteto, amefariki dunia darasani baada ya kudaiwa
kuchapwa viboko na walimu watatu wa shule hiyo, kwa kile kilichodaiwa
kufeli mtihani wa Kiswahili.
Polisi wilayani na mkoani Manyara, wanamshikilia mwalimu mmoja baada ya wenzake kukimbia baada ya tukio.
Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samwel
Nzoka alimtaja mwanafunzi huyo aliyepoteza maisha kuwa ni Noel Bichima
(15).
Kanali Nzoka alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi
wakiwa darasani, wakati mwalimu huyo anayeshikiliwa na polisi alipokuwa
akiwafundisha. Inadaiwa mwanafunzi huyo alichapwa viboko vinane.
Haikuelezwa kama alichapwa kiganjani ama sehemu nyingine.
Nzoka alidai kuwa mwalimu huyo alimchapa marehemu baada ya
kupata alama 40 katika mtihani wa somo la Kiswahili kwani walipeana
mkakati wa kutofeli na kwamba mwanafunzi atakayepata chini ya alama 40
atachapwa fimbo 12.
“Mwanafunzi huyo alifariki dunia papo hapo darasani
baada ya kuanguka chini alipochapwa viboko na walimu hao na mwili wake
umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ukisubiri uchunguzi,” alisema Kanali Nzoka.
“Natoa wito kwa walimu wa shule za msingi na sekondari,
kuangalia namna ya kutoa adhabu kwa wanafunzi wanapokosea, baadhi ya
watoto afya zao siyo nzuri,” alisema Kanali Nzoka.
Diwani wa Kata ya Matui, Athumani Kidawa alisema baadhi ya
wazazi wa eneo hilo waliopatwa na hasira baada ya kutokea tukio hilo,
waliandamana hadi Kituo cha Polisi Matui kulalamikia kitendo hicho.
0 comments:
Post a Comment