Wimbo na video ya mpya ya Vanessa Mdee ‘Nobody But Me’ ni kitu
ambacho kitakuwa ni kosa kama sisi tunaochambua muziki tukinyamaza na
kutoisema dhahabu iliyomo kwenye wimbo huo.
Nilikuwa kwenye redio kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kuingia kwenye
uandishi wa masuala ya burudani huu ukiwa ni mwaka wa tatu sasa. Hiyo
inamaanisha kuwa kwa zaidi ya miaka 13, sikio langu limekuwa
likisikiliza nyimbo nyingi sana za kila kona ya dunia.
Kwa miaka hiyo yote nimekuwa nikisikiliza nyimbo si kama msikilizaji
wa kawaida, bali kama jaji kama wale wanaoshirikishwa kwenye mashindano
ya muziki duniani.
Wakati mwingi sana pamoja na kuzijaji nyimbo mpya zinazotoka,
nimekuwa nikiyatunza tu maoni yangu moyoni au labda kuyashirikisha kwa
wenzangu wa Bongo5.
Lakini mara nyingi nimekuwa na desturi ya kuchukua muda na kuandika
kitu pale ninapoona kazi nzuri ya kutolewa mfano. Nobody But Me imenipa
mzuka huu wa kutonyamaza bali kuusema uzuri wake.
Well, unajua sasa hivi muziki wa Tanzania umebadilika mno. Si ule
kama wa zamani ambapo nyimbo kama Mabinti, Cheza Kwa Step, Ghetto Langu,
CNN na zingine tulizokuwa tukiziskia kwenye vipindi vya mchana vya
redio zetu pendwa.
Nyimbo nyingi sasa hivi ni zile zinazokulazimu ukimbie nazo na wakati
mwingine zinakuwa ni kama chotara wa Bongo Flava na muziki wa Nigeria.
Ndio maana nyimbo zenye ladha ya ‘Nobody But Me’ ni chache mno
kuzisikia.
Kwahiyo kwa Vanessa kufanya wimbo wa R&B, mahadhi ambayo ni kama
‘endangered species’ kwenye redio, hatuwezi kukaa kimya bila kumpa
pongezi zake ili muda, nguvu, ubunifu na gharama alizotumia kutengeneza
‘this masterpiece’ zisionakane kama ni bure tu.
Nobody But Me ni ngoma kali. Ni kabila moja na collabo zenye
mchanganyiko wa R&B na Hip Hop kama zile ambazo Beyonce amekuwa
akizifanya na mume wake Jay Z. Narudia tena kwamba real recognize real’
kwa maana kwamba kama wewe ni mtu unayesikiliza muziki juu juu tu
unaweza usielewe hiki ninachokisema.
Vanessa ni genius! Kumwimbisha Kiswahili mtu anayetajwa kuwa rapper
namba moja ama namba mbili Afrika Kusini si kitu cha kubeza! Nobody But
Me ni wimbo ulioandikwa na kutayarishwa vizuri unaochezeka na
kusikilizika vizuri ukilinganisha na nyimbo nyingi za sasa ambazo nyingi
zimekuwa ni za kuchezeka zaidi kuliko kusikilizika.
Kwa haraka haraka title ya wimbo inaweza kukufanya udhani kuwa
Vanessa angeimba Kiingereza peke yake, lakini kwa kutambua kuwa muziki
ni lugha ya dunia, ameamua kukipaisha Kiswahili, lugha yetu ya taifa.
Unaweza kusikia jinsi ambavyo Vee Money ameendelea kupevuka kiuimbaji
siku hadi siku na nidhamu yake kwenye kazi hiyo haielezeki.
Video ya Nobody But Me ni kitu kingine kinachoufanya wimbo huu uwe
tofauti na zingine na uwe si wimbo tu mkali kwa Tanzania, bali ni wimbo
mkali kwa Afrika. Ni video ya kujiachia yenye mandhari tofauti na
isiyochosha kuitazama. Ni aina ya video tulizozoea kuziona zikifanywa na
wasanii wakubwa wa Marekani.
Kuna haja ya kuzungumzia uchaguzi bora wa nguo zao kwenye video hiyo?
Hakuna shaka kwa video hiyo, Vanessa Mdee ni msanii bora wa kike
Afrika Mashariki kwa sasa. Vanessa anawafundisha wasanii wengine wa
Afrika Mashariki kuthubutu kwa kufanya nyimbo tamu za Kiswahili zenye
sura ya kimataifa.
Vanessa anaipeperusha bendera ya Tanzania kwa nguvu zake zote. Ni
muhimu kutambua jitihada zake hizo na kukipongeza kipaji chake.
Kwakuwa ni nyimbo chache kali zenye mahadhi ya R&B na Hip Hop kwa
pamoja tangu mwaka 2015 uanze, Nobody But Me haina mpinzani na kwakuwa
ni wimbo ulioikutanisha Tanzania na Afrika Kusini, unaufanya kuwa wimbo
mkubwa zaidi katika robo hii ya kwanza ya mwaka.
Swali la kama wimbo huo kamuimbia Jux (kitu ambacho kina uwezekano mkubwa) nalihifadhi kwaajili ya siku nyingine!
0 comments:
Post a Comment