Wednesday, April 22, 2015

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM Chazidi Kujipatia Sifa Chaingia Kumi Bora ya Vyuo Bora Africa


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeshika nafasi ya kumi miongoni mwa vyuo vikuu 50 bora na vyenye umaarufu Afrika.

Kadhalika UDSM kimetajwa kuwa miongoni mwa chuo vikuu chenye idadi kubwa ya wanafunzi na walimu na wingi wa programu za masomo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema chuo hicho kina haki ya kushika nafasi hiyo kutokana na jitihada zinazofanywa na uongozi.

“Tulifanya jitihada kuhakikisha tuna walimu wazuri wenye shahada za uzamili na uzamivu, maabara nzuri na miundombinu rafiki ya kufundishia,” alisema Mukandala.

Alisema UDSM ina mitaala bora inayoendana na wakati na inazalisha wataalamu wengi kwa mwaka.

“UDSM inachaguliwa na wanafunzi wengi na pia ina wanafunzi wa kimataifa,”alisema.

Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Vyuo Vikuu na vya Kati (4ICU) ya Uingereza, chuo hicho kilishika nafasi ya 10 kati ya vyuo 50 vilivyopimwa kulingana na vigezo vya taasisi hiyo.

Hata hivyo, taasisi hiyo ilieleza kuwa hawapimi ubora wa vyuo kwa kuangalia kiwango cha elimu inayotolewa au huduma bali wanaangalia umaarufu wa chuo kimataifa.

“Huu mtandao si kwa ajili ya taaluma wala usichukuliwe kama kipimo cha kuchagua programu au nafasi ya masomo, huu ni kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa kimataifa kufahamu jinsi taasisi ya elimu ilivyo maarufu katika nchi nyingine,” ilisema taarifa ya 4ICU.

Katika taarifa hiyo, Chuo Kikuu cha Cape Town cha Afrika Kusini kilishika nafasi ya kwanza huku vingine vilivyoshika tano bora vikitoka nchini humo.

Nafasi ya pili ilishikwa na Chuo Kikuu cha Pretoria, ya tatu Chuo Kikuu cha Stellenbosch na nne ilikwenda kwa Chuo Kikuu cha Witwatersand na tano ikishikwa na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.

Ikieleza namna walivyoweza kupata vyuo bora, tovuti ya 4ICU iliangalia jinsi mitandao mingine inavyozungumza na kutoa taarifa za chuo husika, nafasi yake katika kurasa za mtandao ya kijamii kutafuta taarifa kwa google, chuo kinavyotumiwa kama rejea katika taarifa mbalimbali na ni kwa kiasi gani watu wanaitumia tovuti ya chuo husika

0 comments:

Post a Comment

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More